Na Tegemeo Kastus
Mwenyekiti wa bodi ya afya ameitaka timu ya usimamizi ya afya wilaya ya Karatu kumsaidia Mganga Mkuu wa wilaya kwa kumpa taarifa za vituo vyote vya afya. Hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji katika idara ya afya na kusaidia kutatua changamoto kwa wakati.
Mwenyekiti ndugu Joseph Fisso amesema hayo wakati bodi ya afya na wajumbe wake walipokaa kikao katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu. Ndugu Fisso ameomba wajumbe kuendelea kushikamana na kuimarisha huduma za afya. Amesema mgawanyiko wa wafanyakazi wa afya kipindi cha nyuma ulisababisha huduma za afya kutoridhisha, kwa sasa mgawanyiko hakuna na huduma zinaendelea kuimarika siku hadi siku. Madaktari wamezidi kutoa huduma nzuri kwa wananchi na ameombwa watendaji wa chini wa afya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Ndugu Fisso ameomba Mganga Mkuu kuwa mkali kwa watendaji wa chini yake. Amesema utatuzi wa changamoto za afya siyo rahisi kama watu wa nje wanavyofikiri, kuna ugumu wake lakini tunaweza kutumia timu ya usimamizi wa huduma za afya kufanya ukaguzi wa afya kwa kila kituo cha afya. Amesema timu ya usimamizi wa huduma za afya ikifanya kazi vizuri, na ikatoa taarifa za kutopatikana kwa dawa kwa wakati zitamfikia Mganga Mkuu mapema na kufanyia kazi.
Naye Dkt Mustafa Waziri Mganga Mkuu wa wilaya amesema kuna mambo yamefanyika mazuri, amesema kuna wafanyakazi wa idara ya afya 89 wamepandishwa madaraja. Amesema ukusanyaji wa damu wilaya ya Karatu umeongezeka sana na imekuwa ni Halmashauri inayoongoza katika ukusanyaji wa damu kuliko wilaya nyingine za mkoa wa Arusha.
Wajumbe wa bodi ya afya wakiwa katika kikao ukumbi wa Halmashauri
Dkt. Mustafa waziri amesema azimio la kwanza katika kikao hicho cha bodi ya afya ya wilaya ni kuitisha kikao cha wadau wa afya juu ya upatikanaji wa dawa za kunyunyizia katika maeneo mbalimbali Karatu ili kuchukua tahadhari ya virusi vya ugonjwa wa corona. Amesema azimio la pili kuhakikisha kila kituo cha afya au zahanati eneo la mipaka yake inapimwa ili kuondoa migogoro ya ardhi. Azmio la tatu ni kupanga dawa na kubandika orodha ya dawa zinazopatikana kwa kila kituo cha afya na zahanati. Azimio la nne ni kufanya ukaguzi wa dawa kwa kila kituo na zahanati. Azimio la mwisho ni kuandaa madeni ya MSD kwa kila kituo kinachodaiwa na kuwapa mda wa kulipa.
Dkt, Heriel Zacharia Mganga Mfawidhi Hospitali teule ya wilaya (CDH) amesema fedha million 59 wanazopata kutoka serikalini (basket Fund) kwa kila robo wanatumia mgawanyo million 40 kwa ajili ya dawa na kiasi kinachobakia kinatumika kwa ajili ya mafuta ya ambulance na malipo ya watu wanaopeleka vifaa. Dkt. Zakaria amesema hospitali teule ya wilaya ina wastani wa kupokea watu wa bima ya afya takriban 700 mpaka 800 kwa mwezi. Dkt. Zakaria amesema fedha za serikali zinatumika vizuri ila changamoto ipo kwa watu wa bima ya afya na fedha nyingine zinazoingia kama ruzuku zianachelewa kulipwa kwa wakati.
wajumbe wa bodi ya afya wilaya katika matukio mbalimbali kwenye Kikao.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa