Kikao maalumu cha kamati ya ushauri wilaya kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri, na kuongozwa na Mwenyekiti Mhe. Theresia Mahongo. Kikao hicho ambacho jukumu lake ni kushauri kilifanya mapitio ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha na kuridhia kupitisha bajeti hiyo.
Mwenyekiti wa Kikao hicho Mhe. Mahongo amewapongeza watendaji wa Halmashauri kwa kuandaa bajeti bora iliyokidhi mahitaji ya kila sekta. Amesema upangaji wa bajeti mwaka huu umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Makadirio ya bajeti ya fedha mwaka ujao ni takribani shilingi billion 3.9 tofauti na makadirio ya sasa ambayo ni shilingi billion 3.3. Mhe. Mahonngo amepongeza Halmashauri kwa kufika kiwango cha 50% ya ukusanyaji wa mapato kwa robo iliyomalizika ya mwaka huu wa fedha amesema hiyo ni ishara njema. Amesema fedha za mapato ndizo zinatolewa na serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhe Mahongo amesema anataka mapato ya mwakani yafike kiwango cha billion 4, Karatu kuna vyanzo vingi sana vya mapato lakini bado hatuvitumii vizuri. Amesema mathalani ziwa Eyasi watu wanavua samaki kinyemela na kusafirisha lakini hakuna mapato yanayopatikana. Amempa Malekezo Afisa mifugo kwenda kushughulikia changamoto hiyo mapema iwezekanavyo kabla hajachukua hatua kali zaidi.
Mwenyekiti Mhe. Mahongo amesema juzi usiku kikosi kazi kimekamata ndoo 20 jana usiku wamekamata ndoo77 za samaki ambazo hazijalipiwa ushuru. Amesema hawezi kuvumilia upotevu huo wa mapato katika eneo lake. Ameelekeza mashine za malipo kwa njia ya mtandao POS zipelekwe Mang’ola na Afisa tarafa pamoja na Afisa mifugo washirikiane kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali. Njia zote zinazoaminika samaki wanapitishwa wawekwe watu ili kuhakikisha stakabali zinatolewa na watu wanakuwa huru kuendelea na shughuli zao za uvuvi wa samaki.
Maafisa uchumi wa Halmashauri ya Karatu kushoto wakifutatilia kwa makini mapitio ya bajeti ya fedha kifungu kwa kifungu.
Mhe. Mahongo ameelekeza Afisa mifugo kuhakikisha hakuna uvuvi haramu unaofanyika kwa kutumia kokoro. Uvuvi ambao unaharibu mazalia ya samaki wadogo, amewataka kujipanga na kutoa taarifa za utekelezaji wa maelekezo yake. Lakini pia kuwapa uhuru wananchi kujihusisha na shughuli za uvuvi kwa sababu ziwa limejaa maji na lina samaki wengi kwa sasa.
Mhe. Mahongo ameonesha kusikitishwa na utoro wa wanafunzi katika kata ya Kansay baada ya kupokea taarifa ya watoto 80 ambao hawajajiunga na kidato cha kwanza katika na shule ya sekondari Kansay. Amemuelekeza mtendaji wa kata ya Kansay kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha watoto hao wamejiunga na elimu ya sekondari. Amesema shule ya Kansay ina madarasa ya kutosha baada ya kukamilika jengo la utawala, amesema awali walimu walikuwa wanatumia vyumba viwili vya madarasa kama ofisi ambavyo sasa wanafunzi wanavitumia.
Mhe. Mahongo ameasa wananchi kutocheza na elimu, amewaelekeza watendaji wachukue hatua kali kwa wazazi walioshindwa kupeleka watoto shule. Amesema wiki ijayo atakuwa na ziara Kansay kufuatilia chanzo cha tatizo hilo, ameomba viongozi wa dini kumsaidia kutoa elimu ya ufahamu kwa wananchi juu ya umuhimu wa elimu. Amesema maendeleo hayana lelemama, kwa sasa hatuwezi kueleweka ila baadae ndio tutaeleweka tunachosisitiza. Bila ya elimu tumekwisha tukipata elimu maradhi yatakwisha, umasikini utakwisha, amesema tukicheza nayo tutaumia. Ametoa maelekezo kwa wakuu wa sekondari kuhakikisha hakuna mtoto atakayeshindwa kwenda shuleni kwa kisingizio cha kukosa sare za shule. Amesema wanafunzi wasio na sare watumie sare za shule ya msingi na waendelee na masomo.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa