NA TEGEMEO KASTUS
Wananchi lazima tuwe na ari ya kuanzisha na kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yetu. Tukijiwekea mikakati ya kujenga zahanati lazima vitendo vyetu vitafsiri malengo ya kuwa na zahanati, hata wadau wa maendeleo wanapokuja kutusaidia basi wakute tumeshaanza ujenzi.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda katika kikao cha ndani na wazee wa kimila (Malagwanani) huko Lositete. Amesema serikali imetoa kiasi cha Million 150 wilaya ya Karatu kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma katika zahanati ya Jobaj, Mang’ola juu, na zahanati ya Huduma. Zahanati zote hizo zimejengwa na vijiji husika amesema mpaka sasa kuna zahanati tano wilayani Karatu ambazo ni Bashay, G-arusha, Sumawe Mahhahha na Marera tayari zimeshakamilika na zinasubiria kufunguliwa baada ya kumaliza usajili. Ameongeza kusema Wilaya ya Karatu inapata bajeti million 450 kutoka serikalini kwa ajili ya madawa kila mwaka.
Mh. Abbas Kayanda akiwa katika kikao cha ndani na wazee wa kimila.
Akizungumzia kuhusu usambazaji wa umeme vijijini Mh. Kayanda amesema serikali imevunja mkataba na mkandarasi wa awali wa usambazaji wa umeme (REA three) round one ambaye alitakiwa kumaliza kazi tarehe 30 mwezi wa nane baada ya kushindwa kuendana na makubaliano ya mkataba. Hivi sasa Tanesco inafanya tathimini ya mradi mzima ili waweze kumalizia, maeneo yaliyobakia, amewahakikishia wazee wa kimila wa Lositete kwamba umeme utafika Lositete kwa sababu kijiji cha Lositete kipo ndani ya Mpango wa kusambaza umeme. Amesema vijiji ambavyo havikuingia kwenye awamu hii vitawekwa kwenye umeme wa (Rea three round two) na utasambazwa kwenye taasisi zote za serikali kama shule zahanati na ofisi za kijiji.
Kuhusu barabara Mh. Kayanda amesema barabara ya Lositete lazima itakarabatiwa kwa sababu tayari iko kwenye bajeti ya mwaka huu. Utengenezaji wa barabara za vijijini unasimamiwa na wakala wa barabara vijijini (Tarura) Mh. Kayanda amewashukuru wazee wa kimila kwa kudumisha hali ya ulinzi na usalama. Amesema wazee wamekuwa imara kuwaelekeza vijana mambo ambayo serikali inawahitaji kufanya.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wananchi wa Lositete
Pamoja na kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Kayanda alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Lositete ambao walikuwa katika mkutano wao mkuu wa kijiji. Pamoja na mambo mengine amewahidi kuendelea kushirikiana nao amesema uongozi si kuongoza peke yako lazima kushirikiana na wananchi katika kuongoza.
Awali katika salamu zao wazee wa kimila walimueleza Mkuu wa wilaya furaha yao kwa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu ndg. Waziri Mourice aliyewaahidi wanakijiji wa Lositete kiasi cha million 7.7 kwa ujenzi wa matundu ya vyoo shule ya msingi Lositete, ukarabati wa majengo matatu ya nyumba za walimu na kukubali kuwalipia mshahara walimu wa ziada wapatao wanne wa muda wa miezi miwili mwezi November na Desember.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa