Na Tegemeo Kastus
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo amewapongeza wajumbe wa Mamlaka ya mji mdogo waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kipindi cha miaka mitano. Wajumbe hao walikutana katika kikao cha kwanza cha Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo kilichofanyika Ukumbi wa Halmashauri.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza la mji mdogo Mhe. Mahongo amewaomba wajumbe hao wa Mamlaka ya Mji mdogo kujikita katika kulinda ulinzi na usalama. Amesema Karatu ni kitovu cha utalii lazima tuimarishe mazingira ya ulinzi na usalama. Wageni wakija na kurudi salama biashara ya utalii itaongezeka na kipato chetu sisi wananchi kitaongezeka.
Mhe. Mahongo amesema kuna miradi viporo ambayo inapaswa kumalizika tarehe 30 mwezi wa 6 mwaka 2020. Amesema hayo ni maelekezo ya serikali, Mh. Mahongo amesema kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi aliyofanya ameona kasi ya ukamilishaji wa miradi viporo hairidhishi hivyo ameelekeza wajumbe wa mamlaka kwenda kuongeza kasi katika umaliziaji wa miradi viporo. Mhe. Mahongo amepongeza kukamilika kwa zahanati ya G-Arusha iliyoanza kipindi cha nyuma sasa imebakiza ujenzi wa choo cha nje. Mhe. Mahongo ameelekeza wataalamu wa afya wapelekwe wakati utekelezaji ujenzi wa choo ukiendelea. Amesema hiyo italeta faraja kubwa kwa wananchi kuanza kupata huduma za afya katika zahanati yao.
Mhe Mahongo ameomba wajumbe wa mamlaka ya mji mdogo kujikita katka usafi wa Mazingira katika maeneo yao. Amesema kuna miti ya Minyaa mirefu ambayo inahatarisha usalama wa maisha ya watu. Amesema urefu wa Mnyaa kwenda juu haupaswi kuzidi mita moja kwenda juu, usafi wa mazingira utatupunguzia maambukizi ya maradhi mbalimbali. Amesema tukienda vizuri kuna zawadi ya usafi wa mazingira zinazotolewa na serikali katika maeneo yanayofanya vizuri kwa usafi. Amepongeza Lotari klabu kwa kutengeneza dastibini 21 zenye thamani 2100,000 zilizotengenezwa kwa gharama zao. Wametengeneza Dastibini ili wananchi watumie kutupa taka katika sehemu zilizowekwa.
wajumbe wa Mamlaka ya mji mdogo wa Karatu wakiwa katika kikao cha baraza.
Mhe. Mahongo ameomba wajumbe waliochaguliwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato. Amesema hicho ni moja ya kigezo kitakachopimwa ili kuweza kutoka kwenye mamlaka ya mji mdogo na kupata hadhi ya kuwa Mji. Amesema kama tuna uwezo wa kujitegemea inakuwa ni jambo rahisi.
Mhe. Mahongo ameomba wajumbe wa Mamlaka ya Mji mdogo kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa virusi vya corona, amesema ni vyema viongozi kutoa elimu kwa wananchi kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ya madaktari na maafisa afya. Amesema ameshatoa maelekezo kwenye maeneo yote ya biashara kuwekwa ndoo za maji na sabauni ili wananchi wanawe mikono kabla kupata huduma na kufuata kanuni za afya. Mhe. Mahongo amesema maelekezo hayo yatekelezwe kwenye Magulio, kuwe kuna sehemu za kunawa mikono za kutosha ili kuepusha msongamano.
Awali Katika kikao cha baraza la Mamlaka ya mji mdogo Karatu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama pekee kilichotoa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti. Wajumbe wa kikao hicho walipiga kura za siri za ndio au hapana. Ndg. Abbas Kayanda Katibu tawala wa wilaya alisimamia uchaguzi wa Mwenyekiti kwa kutumia kanuni ya 6 kifungu cha 2 na alimtangaza Ndg. Yuda Morata Male kuwa Mwenyekiti wa Mamalaka ya mji mdogo. Ndugu Kayanda alisema Morata alipata kura 31 kati ya kura 36 kura za hapana 3 na kura 2 ziliharibika.
Ndugu. Kayanda alitoa rai kwa wajumbe kwamba kumaliza uchaguzi ni jambo moja, ameomba wajumbe pamoja na watendaji kumpa ushirikiano Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo ili aweze kutimiza majukumu yake vizuri. Amesema matarajio ni kwamba Karatu itatoka kwenye Mamlaka ya Mji mdogo, baada ya miaka mitano na kuwa Halmashauri ya mji wa Karatu.
Kikao hicho kilimchagua makamu Mwenyekiti wa mji mdogo ambaye ni Ndg. Ally Jamal Ally kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mji mdogo. Ndugu Ally alipata kura 35 za ndio kati ya kura 36 na alipata kura 1 ya hapana hivyo kutangazwa mshindi wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Karatu.
wajumbe wakifuatilia kikao cha Baraza la Mamlaka ya mji Mdogo wa Karatu.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa