NA TEGEMEO KASTUS
Mradi wa ujenzi wa choo cha shule ya msingi Bashay uliojengwa kwa nguvu za wananchi na Zahanati ya Bashay inayoendelea kujengwa na TASAF itachunguzwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa. Ili kujiridhisha kama fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa Miradi hiyo zinaendana na thamani ya ujenzi wa majengo yaliyojengwa.
Mh. Abbas Kayanda akikagua mradi wa ujenzi shule ya msingi Bashay
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda aliyeambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, alipotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo. Mh. Kayanda ameoneshwa kutoridhishwa na umaliziaji wa ujenzi wa mradi wa zahanati ya Bashay kwa fedha ambazo zimetolewa na Tassaf. Licha ya uchunguzi kufanyika Mh. Kayanda amemuelekeza fundi anayesimamia ujenzi wa zahanati hiyo kuhakikisha dosari zilizojitokeza katika umaliziaji wa ujenzi wa mradi huo anazirekebisha kwa gharama zake. Ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unakamilika na kuukabidhi kwa mujibu wa makubaliano tarehe 19 mwezi wa tisa. Mh. Kayanda ameelekeza ujenzi wa jengo la mama na mtoto uanze haraka, ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati hiyo utajengwa kwa nguvu za wananchi.
Mh. Abbas Kayanda akikagua ujenzi wa zahanati ya Bashay
Mh. Kayanda ametembelea na kujionea ujenzi wa choo cha matundu 12 katika shule ya Msingi Bashay ambao umegharimu takribani million tisa. Mh. Kayanda ameonesha kutoridhishwa na thamani ya ujenzi wa jengo hilo ukilinganisha na kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya ujenzi. Sambamba na mradi huo wa ujenzi Mh. Kayanda ametembelea eneo linalotarajiwa kujengwa Vyumba viwili vya madarasa kwa fedha zilizotolewa na serikali kupitia mfuko wa EP4R. Ujenzi wa madarasa hayo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha siku 90, Mh. Kayanda ametoa rai kwa watendaji kusimamia vizuri ujenzi wa madarasa hayo kwa kuzingatia muda uliowekwa na lakini kuhakikisha ujenzi wa majengo hayo unaendana na thamani ya fedha zilizotolewa.
Mh. Abbas Kayanda ametembelea na kukutana na wajumbe wa kamati ya ujenzi wa zahanati ya Sumawe
Wakati huo huo Mh. Kayanda ametembelea ujenzi wa zahanati ya Sumawe ambayo ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2011. Ameelekeza watendaji wa kuhakikisha ujenzi wa jengo la zahanati pamoja na ujenzi wa choo unakamilika ifikapo tarehe 30 mwezi wa tisa. Mh. Kayanda amemuelekeza Mganga mkuu wa wilaya kuhakikisha anaanda watumishi wa afya wa kuwapelekeka zahanati Sumawe pamoja na zahanati ya Bashay ili wananchi waanze kupata huduma za afya karibu na maeneo yao wanayoishi. Lengo likiwa ni kuondoa kadhia ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa