Na Tegemeo Kastus
Vikao vya ujirani mwema tunavyokaa ni lazima viwe vina matokeo chanya kwa maslahi ya umma, na maazimio yanayowekwa yanapaswa kutekelezwa kwa wakati. Vikao vya uelimishaji vifanyike kwa wananchi ili kujenga uelewa wa pamoja juu ya namna ya kukabiliana na wanyama pori wanaoingia katika makazi ya watu. Haya ni mambo yatakayowezesha wananchi kuwa na uelewa mkubwa wa sheria na sera za kuhifadhi wanyamapori katika maeneo yanayozungukwa na hifadhi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akiongoza kikao cha ujirani mwema kama Mwenyekiti wa kikao kati ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na watendaji na viongozi wa kata zinazopakana na hifadhi ya Ngorongoro katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu. Amesema vikao vya ujirani mwema lazima vilete mabadiliko ndio maana tunakaa vikao vya ujirani mwema vya wilaya zinazozunguka hifadhi ya Ngorongoro vinavyohusisha viongozi mbalimbali wa wilaya pamoja na wawakilishi wa wananchi. Lengo la vikao vya ujirani mwema ni kujenga mahuiano kati ya jamii na watendaji wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na wajumbe wa mkutano wa ujirani mwema
Mh. Kayanda amesema mapito ya wanyama pori yamefungwa na binadamu kutokana na shughuli za kibinadamu kama kujenga makazi na shughuli za kilimo.Hali inayosababisha wanyama pori kushindwa kupita katika njia zao za asili. Ameongeza kusema katika vikao vya ujirani mwema elimu ni jambo la msingi sana kwa wananchi ili waweze kujua lipi ni sahihi kulifanya na lipi sio sahihi kulifanya.
Mh. Kayanda amesema lazima watendaji wa serikali waweke mikakati ya kuwalinda wanyamapori na kukabiliana na vitendo vya ujangili. Wananchi watoe taarifa kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili ambavyo vinaweka doa katika mahusiano kati ya hifadhi na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi. Mh. Kayanda amesema serikali inathamini na kutambua mchango wa hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ambayo imekuwa ikitoa kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo. Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ni hifadhi inayonufaisha taifa lakini sisi tulio karibu na tunanufaika zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu ndg. Waziri Mourice ameshukuru Mamlaka ya hifadhi za Ngorongro kwa kuunga mkono katika shughuli za maendeleo. Ameomba mamlaka ya hifadhi iendelee kusaidia Halmashauri ya wilaya ya Karatu kwa kuiweka kwenye bajeti. Jambo ambalo litaongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kikao cha ujirani mwema
Afisa maendeleo ya jamii ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Ndg, Nakuroi Parpekin amesema mikakati ya kuimarisha kati ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na wilaya ya Karatu ni pamoja na kuanzisha mchakato wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji vilivyojirani na hifadhi, mkakati ambao utasaidia kuondoa na kupunguza muingiliano wa wanyamapori kwenye makazi ya watu. Amesema sambamba na hilo makakati mwingine ni kushirikiana na wananchi katika vikundi ili kujihusisha na ufugaji wa nyuki ambao utasaidia kuzuia wanyama wasiinge kwenye makazi ya watu.
Ndg. Parpekin amesema Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro wataendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwenye vijiji jirani na hifadhi ya Ngorongoro kama njia moja wapo ya kujenga uelewa kwa wananchi ili waweze kuchukua tahadhari. Ameongeza kusema Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongo itaendelea kuimarisha mahusiano mema na wananchi kwa kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo ya maji afya na elimu.
Naye diwani wa kata ya Oldean. Mh. Peter Masay akichangia katika kikao hicho cha ujirani mwema amesema lazima mamlaka ije na mikakati ya kisera kwa kurekebisha sehemu zenye mapungufu kwa kuziangalia upya na kufanya mapitio upya ya sheria za mamlaka ili kuimarisha dhana ya ujirani mwema. Amesema kuna mambo yanawabana Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kutokana na sheria zilizowekwa hivyo kushindwa kutekeleza baadhi ya mambo.
Wajumbe wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa kikao wakati akizungumza katika kikao cha ujirani mwema.
Amesema lazima mamlaka waje na sera zinazoshabihiana moja kwa moja na dhana ya ujirani mwema, ambayo itasaidia kuimairisha mahusiano yao na wananchi. Amesema kuhusu wanyama wanaoingia kwenye makazi ya watu lazima kuwe na mpango wa muda mrefu na mpango wa muda mfupi. Maisha yanabadilika tusibaki kwenye kutumia njia za zamani za kukabiliana na changamoto hizi, tujifunze wenzetu katika nchi zilizoendelea wanatumia mbinu gani kukabilina na wanyamapori. Amesema mathalani kuweka vifaa vya kutoa taarifa pindi inapotokea wanyamapori wanataka kuingia kwenye eneo la makazi ya watu itasaidia askari kuwadhibiti kabla hawajafanya uharibifu.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa